Serikali imesema kuwa kupitia
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kufanya tathmini ya mahitaji
ya ujenzi wa Kituo cha Forodha katika Jimbo la Momba, ikiwemo upembuzi
yakinifu, upatikanaji na utambuzi wa eneo, gharama za mradi na utayari
wa nchi jirani.
Hayo yalisemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu
Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Momba, Mhe. Condester Michael Sichalwe,
aliyetaka kujua wakati ambao Serikali itajenga kituo cha forodha katika
Jimbo la Momba mkoa wa Songwe.
Alisema eneo hilo linaangaliwa kwa
kuzingatia ongezeko la shughuli za biashara na umuhimu wake katika
kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa biashara
mipakani.
’’Ujenzi wa vituo vya forodha, ikiwemo katika Jimbo la
Momba, hufanyika kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali, ukamilifu wa
taratibu na kanuni za kiforodha, utayari wa nchi jirani tunazopakana
nazo, masuala ya kiusalama, upatikanaji wa rasilimali fedha, pamoja na
tathmini ya umuhimu wa eneo husika katika shughuli za biashara za
mipakani,’’ alifafanua Mhe. Luswetula.
Aliongeza kuwa ujenzi wa
kituo hicho utaanza mara baada ya kukamilika kwa maandalizi yote muhimu,
ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa fedha za utekelezaji wa mradi katika
bajeti ya Serikali na kutangazwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Aidha, Mhe. Luswetula alieleza kuwa TRA inaendelea na
maandalizi na itatoa taarifa rasmi pindi ratiba ya utekelezaji wa ujenzi
itakapokamilika na kuielekeza TRA kuharakisha tathmini hiyo ambayo iko
katika hatua za mwisho.
Naibu
Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akijibu swali
la Mbunge wa Momba Mhe. Condester Michael Sichalwe, Bungeni Jijini
Dodoma, aliyetaka kujua wakati ambao Serikali itajenga kituo cha forodha
katika Jimbo la Momba mkoani Songwe.(Picha na Kitengo cha Mawasilino
Serikalini, Wizara ya Fedha)