Hayo yamesemwa leo Aprili 08, 2026, na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, bungeni jijini Dodoma, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Catherine Canute Joachim, katika Bunge la Kumi na Tatu, Mkutano wa Tatu, Kikao cha Nne.
Akijibu swali kwa niaba ya Waziri wa Afya,.Mhe. Mohamed Mchengerwa, Dkt. Samizi amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza zaidi kwenye uboreshaji wa miundombinu ya hospitali, ikiwemo kujenga majengo mapya na kukarabati yale yaliyochakaa.
Aidha, amesema Serikali inaendeleza upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa kama PET/CT Scan, Angio Suite, Cathlab, na CT Scan, sambamba na kuendeleza mafunzo ya kitaaluma kwa wataalamu wa afya ili kuhakikisha huduma zinakuwa za ubora wa kimataifa.
“Serikali pia inaanzisha huduma mpya za ubingwa bobezi na kuhakikisha hospitali zinapata ithibati za kimataifa, na kuzitangaza katika masoko ya kimataifa ili kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi,” amesema Dkt. Samizi.
Takwimu zinaonyesha ukuaji wa utalii wa tiba: katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, wagonjwa 3,018 kutoka nje ya nchi walipatiwa huduma za ubingwa bobezi katika hospitali za rufaa za mikoa, kanda, maalum na taifa.
Aidha, Dkt. Samizi ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika rasilimali watu kupitia Samia Health Super-specialization Program, ambapo wataalamu 1,483 wanafadhiliwa kusomea fani za ubingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kuongeza ubora na uwezo wa hospitali zetu.